Euphrase Kezilahabi kama Mwanafalsafa Kamili: Mifano Kutoka Riwaya ya Mzingile
Abstract
Makala haya yamejikita katika kumtazama Kezilahabi kama mwanafalsafa kamili anayeifanya kazi yake ipasavyo. Tunafanya hivyo kwa kutumia riwaya yake ya Mzingile. Mtazamo huu unaongozwa na ufafanuzi wa Wiredu (1996b) kama anavyorejelewa na Hallen (2002-7) pale anapoitazama kazi ya kifalsafa kama ‘Jitihada zinazotokana na uwezo wa mtu zenye malengo ya kuanzisha sio tu mawazo mapya peke yake, bali pia kuleta madai mengine ya ukweli unaoshikiliwa kuhusiana na asili ya imani zetu. Hii ikiwa ni pamoja na kuzitathmini, kuzipitia upya na hata kuzitengua imani zetu za kale na hivyo kuanzisha mawazo mapya ambayo yanaweza kufanikiwa kupata hadhi ya kuwa kweli.’ Kwa kutumia riwaya ya Mzingile mwandishi wa makala haya anadhamiria kuonesha kuwa Kezilahabi anajipambanua kama mwanafalsafa kamili. Mtazamo wa mwandishi wa makala haya ni kwamba kupitia riwaya ya Mzingile, Kezilahabi amefanikiwa kuwasilisha kwa wasomaji kisanaa, sio tu kile kinachoweza kutazamwa kama madai mapya ya ukweli unaothibitishwa kuhusiana na asili ya imani bali pia kutathmini, kupitia upya na hata kuzitupilia mbali imani za kale ambazo zinachukuliwa kimazoea kuwa ni kweli. Kwa kufanya hivi, anaweza kutazamwa kama aletaye mawazo mapya ambayo yanaweza kufikia au tayari yamefikia kuwa na hadhi ya ukweli katika jamii. Kezilahabi analitekeleza jukumu hili kwa utaratibu kamilifu kama mwanafalsafa aliyefuzu, na ambaye anajua nini kinapaswa kufanywa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Full Text:
PDFRefbacks
- There are currently no refbacks.