Kiswahili katika Kufundishia TEHAMA katika Shule za Msingi nchini Tanzania: Umuhimu na Changamoto zake
Abstract
Ulimwengu wa sasa wa utandawazi umesababisha kuzagaa kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hususani kompyuta na vitumi vyake. Kwa hali hiyo, maendeleo ya sayansi na teknolojia yamesababisha kuenea kwa lugha zinazotumika kwa wingi katika teknolojia hiyo kama vile Kiingereza na Kifaransa na kudumazwa kwa lugha za Kiafrika zinazotumiwa kwa nadra mno. Uwezo wa kutumia media na vitumi vipya vya teknolojia hii kwa ubunifu na uhakiki aghalabu hutegemea umilisi wake. Umilisi wa kidijitali nao ni zao la mafunzo kupitia lugha zoefu ambayo humpa mwanafunzi fursa ya kushiriki kikamilifu. Makala hii ni sehemu ya matokeo ya uchunguzi mdogo uliofanywa katika mikoa ya kusini mwa Tanzania kuonesha ufaafu wa Kiswahili kama lugha rasmi ya kufundishia somo la TEHAMA katika shule za msingi. Matumizi ya Kiswahili kufundishia stadi za msingi za TEHAMA ni hatua ya mwanzo kuelekea kwenye matumizi ya lugha ya Kiswahili kutolea mafunzo ya kiufundi. Aidha, tunatathmini manufaa na changamoto zinazokabili matumizi ya Kiswahili kama lugha ya TEHAMA.