Dhima ya Mianzo na Miisho katika Nathari za Kiswahili za Fasihi ya Watoto: Mifano kutoka Riwaya na Hadithi za Kiswahili za Watoto nchini Tanzania
Abstract
Fasihi ya watoto hutofautiana na fasihi ya watu wazima katika maudhui, fani, mawanda, walengwa na hata umri. Pamoja na kutofautiana huko, bado dhima ya fasihi inabaki ileile ya kufundisha, kuburudisha, kuonya, kuadibu, kurithisha amali za jamii na kadhalika. Wataalamu mbalimbali wa fasihi wakiwapo waandishi, wahakiki, walimu wanaofundisha madarasa ya fasihi na wengineo, wanafahamu kabisa kuwa kazi za fasihi zinatofautiana kwa muundo na hata mitindo. Hawa wanaongozwa na kaida kadha wa kadha zinazotawala kazi hizo. Nathari ni aina mojawapo ya kazi za fasihi ambazo zina kaida zake zinazoitofautisha na aina nyinginezo kama vile ushairi na tamthiliya. Moja ya kaida zake ni kutumia lugha ya mjazo pamoja na kuwa na sifa ya usimulizi au (uhadithi). Pamoja na sifa hizi kazi zote za nathari huwa na mianzo na miisho ambayo huwa na dhima mbalimbali katika kazi hizo. Makala hii inachunguza mianzo na miisho katika nathari za watoto kwa kutumia Nadharia ya Umuundo. Lengo kuu la makala ni kubainisha mianzo na miisho ya nathari za Kiswahili za watoto pamoja na dhima zake.