Uimarishaji wa Ujinsuke katika Fasihi ya Kiswahili: Mifano kutoka katika Hadithi Teule za Kiswahili za Watoto
Abstract
Lengo la makala hii ni kuchunguza namna hadithi za watoto za Kiswahili zinavyoweza kutumika kama njia ya kuimarisha ujinsuke[1] katika jamii ili kubadili mtazamo hasi kuhusu watoto wa kike na wanawake katika jamii ya Tanzania. Data za mjadala za makala hii zimepatikana kwa kusoma hadithi za watunzi wawili ambao ni Hua (2007) na Mwakoti (2009). Kwa kuongozwa na Nadharia ya Mwitiko wa Msomaji katika uchambuzi wa data za makala hii, inabainika kuwa hadithi zinaweza kutumiwa kuwajengea watoto wa kike mtazamo chanya na uwezo wa kufanya mambo mbalimbali ili kuimarisha usawa katika jamii. Hivyo, hadithi ni njia mbadala ya kuhimiza juhudi na ubunifu kwa watoto wa kike ili kuweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa, kiuchumi na kijamii na kuleta mabadiliko katika mila na desturi zoeleka zinazombagua mtoto wa kike.
[1] Ujinsuke ni tafsiri ya neno la Kiingereza femininity.