Mustakabali wa Tungo za Ngonjera katika Fasihi ya Kiswahili

Authors

  • Esther J. Masele University of Dar es salaam

Abstract

Ngonjera katika kipindi cha kabla na baada ya ukoloni zilionekana kuwa ni njia bora na rahisi ya uelimishaji wa mambo muhimu ya kisiasa na kijamii. Hata hivyo, kuanzia miaka ya 1990 ngonjera zimeonekana kupoteza kabisa umaarufu wake. Lengo la makala hii ni kujadili chimbuko la ngonjera, umuhimu wake kwa jamii na mambo mbalimbali yaliyosababisha ngonjera kupoteza umaarufu wake. Makala hii ni sehemu ya utafiti uliofanywa na mwandishi kwa wanafunzi walimu wanaosomea shahada ya umahiri katika fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Tanzania ambapo data zilipatikana kwa kutumia njia mbili: udurusu wa nyaraka hasa zile zilizojadili kuhusu ngonjera pamoja na usaili. Utafiti huu ulitumia sampuli lengwa ili kuteua wasailiwa na nyaraka za kudurusiwa. Matokeo ya uchunguzi yanaonesha kuwa matumizi ya ngonjera yameshuka au inaweza kusemwa kuwa hayapo katika ulingo wa fasihi tofauti na aina nyingine za ushairi. Miongoni mwa sababu zilizotajwa kuchangia anguko hilo ni dhana ya kuwa ngonjera ni zana iliyotumika kueneza sera za siasa ya ujamaa na kujitegemea. Dhana hii imechangia kukosekana kwa soko la ngonjera katika kipindi hiki kilichotawaliwa na siasa za vyama vingi, jambo lililowafanya waandishi kutojikita katika utunzi wa ngonjera. Mwitikio huu hafifu umesababishwa na kukosekana kwa msisitizo wa elimu kutoka katika ngazi mbalimbali za elimu pamoja na vyombo vya habari kuhusu umuhimu wa ngonjera. Mwisho makala imeshauri njia mbalimbali zinazoweza kuhuisha matumizi ya ngonjera ikiwa ni pamoja na kuingiza ngonjera katika mitaala ya elimu ili ziweze kutumika kama njia ya kufundishia mada zinazohitaji mdahalo. Makala hii imejifungamanisha zaidi kwa mtunzi maarufu wa ngonjera, hayati Mathias Eugen Mnyampala katika mifano na majadiliano.

Downloads

Published

2016-02-13

Issue

Section

Articles