Makosa ya Kiamali katika Kutafsiri Vihisishi: Mifano ya Tafsiri kutoka Kinjeketile (1969) na Amezidi (1995)

Authors

  • Nahashon A. Nyangeri University of Dar es salaam

Abstract

Makosa kuhusiana na tafsiri ya vihisishi aghalabu huwa ni ya kiamali zaidi kuliko kuwa ya kiisimu. Kwa hiyo, mfasiri hana budi kuhakikisha kuwa makosa ya aina hii hayajitokezi kwenye matini lengwa (ML), kwa kuwa hadhira lengwa (HL) huenda ikapata habari za kupotosha. Mfasiri anahitaji maarifa yaliyo zaidi ya uelewa wa kiisimu ili kuibua tafsiri inayofaa. Mara nyingi vihisishi hupewa jukumu la pembeni na wasomi wengi, wakiwamo wafasiri. Inachukuliwa kwamba umuhimu wa kisemantiki, kiamali na wa kimawasiliano kwa jumla wa aina hii ya maneno ni mdogo mno jambo linalosababisha kupuuzwa. Makala inachunguza nafasi ya vihisishi kama aina mojawapo ya maneno yenye umuhimu mkubwa katika kufanikisha mawasiliano katika tafsiri. Mifano kutoka Kinjeketile (Hussein, 1969a) na tafsiri yake ya Kiingereza Kinjeketile (Hussein, 1969b) na Amezidi (Mohamed, 1995) na tafsiri yake He is Far Too Much (wafasiri Weschler na Kimambo, 2012) inaonesha umuhimu wa aina hii ya maneno na changamoto zinazoibuka katika tafsiri. Uchanganuzi linganuzi wa vihisishi katika matini chanzi (MC) na matini lengwa kwa kuzingatia nadharia ya pragmimu au kitendo amali (Mey, 2000; Capone, 2005) unaonesha kwamba mikakati waitumiayo wafasiri si lazima iibue maana kama ilivyo kwenye matini chanzi. Jambo muhimu ni namna ya kuibua athari linganifu kwa misingi ya uamilifu wa matini. Katika hali hii, vihisishi huwa chanzo kikubwa cha makosa ya kiamali. Makala hii inajadili umuhimu huo na jinsi unavyoweza kuzingatiwa katika tafsiri.

Author Biography

Nahashon A. Nyangeri, University of Dar es salaam

Mwalimu

Downloads

Published

2016-02-13

Issue

Section

Articles