Lugha kama Mfumo wa Maana Matinishi: Mfano wa Uamilifu wa Kanuni Geuzaji katika Matini za Sajili ya Mchezo wa Kandanda
Abstract
Jukumu la msingi la lugha kama mfumo wa maana unaowakilishwa kwa maumbo ya kisarufi ni kukidhi mahitaji ya mawasiliano miongoni mwa watumiaji wake. Lugha hupata uamilifu huu baada ya vipashio vyake kupangwa na kuhusishwa na kanuni za kimofosintaksia za lugha hiyo. Upangilifu huu ndio unaozalisha matini zenye usarufi, ukubalifu na mshikamano na ambazo hujitosheleza kimaana. Kanuni Geuzaji huamilishwa kimofosintaksia kwa mujibu wa jinsi elementi za tungo zinavyopangwa kwa njia anuwai ili kuzalisha matini husika. Makala hii inachukua mkabala unaoangalia lugha kama mfumo unaotegemea Kanuni Geuzaji ili kuzalisha matini zenye maumbo mbalimbali zinazotosheleza mahitaji ya mawasiliano. Kwa hiyo, makala inadadisi jinsi Kanuni Geuzaji inavyoweza kuamilishwa katika kufuma maana matinishi kutokana na matini za sajili ya mchezo wa kandanda.