Mafundisho ya Iktibasi katika Utenzi wa Mtu Ni Utu wa Ahmad Nassir Juma Bhalo (Ustadh Bhalo)
Abstract
Tumekuwa tukishuhudia matukio kadhaa ya kutoweka kwa utu miongoni mwa wanajamii duniani. Hata hivyo, kuna kazi za kifasihi ambazo zinashadidia kuenzi hazina hii ya falsafa ya utu ambayo imetawala maisha ya mwanadamu akiwamo Mwafrika. Kwa mantiki hii falsafa ya utu imekuwa ikijitokeza katika kazi nyingi za kifasihi ukiwamo Utenzi wa Mtu ni Utu ulioandikwa na marehemu Ahmad Nassir Juma Bhalo. Azma ya makala hii ni kuchunguza falsafa ya utu katika Utenzi wa Mtu ni Utu kwa kutumia mtindo wa iktibasi ambao ni mkabala unaotumia maandiko kutoka kwenye Kurani na Hadithi za Mtume Mohammad (S.A.W)[1] bila kutaja kwamba unatumia maandiko hayo. Makala hii imedhihirisha kwamba mafundisho yote yaliyoibuliwa katika utenzi huu kama vile tawheed, nasaha, upendo, mazingatio, unyumba, urafiki na zinduko yameandikwa kwa mfumo wa iktibasi. Mfumo huu hutumia Kurani Tukufu na Hadithi za Mtume (S.A.W) bila kusema ni Kurani au Hadithi za Mtume.
[1] Swalallah Alyihi Wasalaam