Upokeaji na Ukubalifu wa Vitamkwa vya Kiarabu na Kiingereza katika Fonolojia ya Kiswahili
Abstract
Makala hii inachunguza jinsi vitamkwa vya kigeni [χ], [ɣ], [ð] na [θ] vilivyopokelewa katika fonolojia ya Kiswahili kutoka Kiarabu na Kiingereza. Lengo la makala hii ni kuelezea sababu za ukubalifu[1] wa vitamkwa hivyo katika mfumo wa fonolojia ya Kiswahili, licha ya mifumo ya fonolojia ya lugha kufikiriwa kuwa thabiti zaidi dhidi ya mabadiliko. Data zilizotumika zilipatikana kutoka Kamusi ya Kiswahili Sanifu (KKS) (2013) Toleo la Tatu na Bosha (1993). Nadharia ya Umbo Upeo imetumika katika uchanganuzi wa data za makala hii. Kuna mikakati ya urekebishaji kadhaa ambayo inaelezea jinsi vitamkwa vinavyoshughulikiwa katika upokeaji wa maneno ya mkopo katika muktadha wa nadharia hii. Hata hivyo, ilibainika kuwa vitamkwa vya kigeni [χ], [ɣ], [ð] na [θ] vilighairi mikakati hiyo ya urekebishaji na kupenyeza katika fonolojia ya Kiswahili. Upokeaji wa vitamkwa hivyo uliwezekana kupitia upangiliaji upya wa mashartizuizi ya Kiswahili katika Umbo Upeo. Vitamkwa vilivyopokelewa vilikubalika katika mfumo wa orodha ya konsonanti za Kiswahili kwa kuzingatia msingi wa iktisadi ya sifa na mvutano pande mbili. Vitamkwa hivyo vilipokelewa kutokana na kuwapo kwa mapengo ya vitamkwa hivyo katika orodha ya vitamkwa vya Kiswahili.