Matumizi ya Methali za Kiswahili kwa Jamii: Mifano kutoka Nchini Kenya
Abstract
Methali hutokana na utamaduni wa watu na hutumika katika kuibulia na kuelekezea busara ya wenyeji. Aidha, methali za Kiswahili zimeshirikisha methali za jamii mbalimbali za Afrika Mashariki. Kwa sababu hii, zina mtazamo unaovuka mipaka ya jamii moja. Kwa hali hiyo, methali za Kiswahili ni mwavuli unaohifadhi na unaoibulia utamaduni asilia wa wenyeji. Methali hizo hutekeleza dhima ya uashiriaji, uelezaji na uelekezaji kuhusu maisha kwa kuzingatia ' undani ' na ' upana ' wa Wakenya kama jamii moja. Data za makala hii zilitokana na methali zilizohifadhiwa katika vitabu vya methali za Kiswahili zilizokusanywa kutoka kwa wanajami wa Kenya. Methali hizo zilipata maelezo ya wanajamii wa Kenya. Kadhalika, wataalamu wa lugha na wahakiki wa fasihi walihojiwa ili kupata fasiri za kijumla kuhusu methali. Katika uchanganuzi wa data, Nadharia ya Semiotiki imetumika kubainishia viashiria na viashiriwa vya kitamaduni katika jamii za Wakenya. Kwa hivyo, makala hii inaeleza namna methali hizo zinavyoweza kutumiwa kwa ufaafu zaidi kwa jamii za Kenya.