Utafiti huu ulichunguza aina za dosari za kisarufi zinazofanywa na wanafunzi wanaojifunza Kiswahili sanifu kama lugha ya pili katika baadhi ya vyuo vikuu nchini Burundi. Data zilikusanywa kutoka kwa wanafunzi wanaosoma mwaka wa pili na wa tatu katika vyuo vikuu husika. Usampulishaji nasibu ulitumika kupata sampuli ya washiriki 80. Data zilikusanywa kwa njia za hojaji na upitiaji nyaraka. Matokeo yalionesha kuwa wanafunzi hufanya dosari mbalimbali za kisarufi katika makundi makubwa manne ya kisarufi ambayo ni: ya kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia na kisemantiki. Dosari hizi zinazotokana na athari za lugha za awali katika Kiswahili sanifu zilidhihirisha hali ya wanafunzi kutoweza kubainisha tofauti kati ya mifumo ya kisarufi ya lugha hizo za awali na ule wa Kiswahili sanifu.