Mawanda ya Taaluma za Ukalimani na Tafsiri na Haja ya Kuboresha Ufundishaji Wake
Abstract
Umuhimu wa ukalimani na tafsiri umeongezeka kutokana na utandawazi. Wakalimani na wafasiri wengi wamekuwa wakiandaliwa ili kuendana na kasi ya ongezeko la mahitaji ya wakalimani na wafasiri. Kutokana na kasi ya ongezeko hili, na uhaba au ukosefu wa walimu wabobevu wa ukalimani na tafsiri, walimu wa lugha ambao tafsiri na ukalimani si nyuga zao za ubobevu wamejikuta wakipewa majukumu ya kufundisha kozi za ukalimani na tafsiri vyuoni. Matokeo yake, walimu hao wamekuwa wakihangaika kufikiria mambo ya kufundisha. Kwa kuwa ukalimani na tafsiri si nyuga walizobobea, hujikuta wakifundisha juujuu. Wahitimu wanaotokana na ufundishaji wa juujuu huwa hawajapikwa sawasawa lakini hutazamiwa kuwa walimu wa baadaye wa ukalimani na tafsiri vyuoni. Aidha, huchukuliwa kuwa wamesomea kozi hizo. Kutokana na kutoandaliwa vyema, hujikuta wanaishia kuchukua miongozo ya kozi waliyotumia enzi za uanafunzi wao. Kisha, huhawilisha kwa kiasi kikubwa yale waliyofundishwa na mwalimu mwanzilishi wa kozi na kuyarithisha kwa vizazi vingine bila kuongezewa vionjo vya kibunifu kuendana na mabadiliko na mazingira ya soko. Hivyo, ufundishaji huwa wa kimazoea zaidi. Kwa hiyo, kuna haja ya wanataaluma kubadilishana uzoefu miongoni mwao, kukumbushana kuhusu mabadiliko yanayotokea na kuboresha zaidi ufundishaji wa nyuga hizi. Makala hii imelenga kutimiza azma hii kwa kujielekeza katika maarifa ya kibiashara kama kionjo kinachohitaji kuongezwa katika mitalaa ya ukalimani na tafsiri vyuoni ili kuboresha ufundishaji wa nyuga madhukura. Hususani, makala inatilia mkazo elimu ya huduma kwa wateja na uandaaji wa nyaraka za kibiashara. Makala inasisitiza kuwa, kutokana na umuhimu wake, elimu ya huduma kwa wateja haina budi kuongezwa katika mitalaa ya ukalimani na tafsiri.