Mtindo wa Uhalisiajabu katika Riwaya ya Kiswahili
Abstract
Mijadala mbalimbali imefanywa na wataalamu na wahakiki wa kazi za fasihi kuhusu mtindo wa uhalisiajabu. Miongoni mwake ni ile inayobainisha chanzo chake katika fasihi ya Kiswahili, athari za matumizi yake, na namna inavyoweza kuakisi hali halisi ya maisha katika jamii husika. Pamoja na mijadala hiyo kuweka misingi katika uelewekaji wa kazi za fasihi zinazotumia mtindo wa uhalisiajabu, suala la aina za mtindo wa uhalisiajabu halijajadiliwa kwa kuzingatia upekee na umuhimu wake. Makala hii imebainisha aina hizo kama zinavyojitokeza katika riwaya za Kiswahili za kihalisiajabu kwa kurejelea mifano kutoka riwaya za Nagona (Kezilahabi, 1990), Bina €“ Adamu! (Wamitila, 2002) na Babu Alipofufuka (Mohammed, 2001). Data ilikusanywa maktabani katika vitabu teule kwa kutumia mbinu ya usomaji wa matini. Uchambuzi, uhakiki na uwasilishaji wa data uliongozwa na Nadharia ya Uhalisia kwa kutumia mkabala wa kitaamuli. Kwa kuzingatia kigezo cha kimaana, makala imebainisha aina sita za uhalisiajabu ambazo ni uhalisiajabu fantasia, tarazi, fifi, wa kimajazi, tashihisi na uhalisiajabu nasibishi.