Dhima ya Miiko katika Uibuaji wa Maudhui katika Fasihi ya Kiswahili: Mifano kutoka Riwaya ya Bw. Myombekere na Bi. Bugonoka Ntulanalwo na Bulihwali
Abstract
Makala hii inajadili dhima ya miiko katika uibuaji wa maudhui katika fasihi ya Kiswahili. Shabaha kuu ni kubainisha jinsi miiko ilivyo na dhima katika uibuaji wa maudhui mbalimbali katika jamii. Makala hii imetokana na madai ya baadhi ya tafiti zilizotangulia kueleza kwamba miiko ni imani za kishirikina (Frazer, 1940; Smith, 1961; Fielding, 1966) na inatumika katika jamii ambazo ziko nyuma katika masuala ya kisayansi (Madumulla, 1988). Kutokana na mitazamo hiyo, tuliona ipo haja ya kuchunguza dhima ya miiko katika uibuaji wa maudhui kwa wanajamii kupitia riwaya ya Kiswahili. Ili kutimiza azma hii riwaya ya Bw. Myombekere na Bi. Bugonoka Ntulanalwo na Bulihwali ilichunguzwa. Uchambuzi wa data uliongozwa na Nadharia ya Ontolojia ya Kiafrika. Matokeo ya uchunguzi katika makala hii yamebaini kuwa miiko katika fasihi ya Kiswahili ina dhima ya kuelezea maudhui mbalimbali. Baadhi ya maudhui hayo ni maadili, mahusiano ya jamii, afya, imani za kijamii, thamani ya kazi na umuhimu wa kutunza mazingira. Miiko hiyo husawiriwa ndani ya jamii na kuakisi uhalisi wa maisha katika miktadha mbalimbali ya kijamii, kiutamaduni, kijiografia na ulimwengu kwa ujumla.