Nafasi ya Biashara za Kimataifa katika Kukuza Uzungumzaji wa Kiswahili kwa Wanafunzi wa Shule za Sekondari Nchini Rwanda
Abstract
Tafiti zinaonesha kwamba lugha ya Kiswahili nchini Rwanda haizungumzwi vizuri kama lugha nyingine zinazofundishwa nchini humo. Ingawa lugha hii haizungumzwi kwa ufasaha, hasa katika shule za sekondari, wanafunzi wanaojifunza katika baadhi ya shule za sekondari wanapata fursa ya kuchangamana na wazungumzaji wa Kiswahili. Wazungumzaji hao ni pamoja na wazazi, jamaa na marafiki wanaofanya biashara za kimataifa za kuvuka mpaka. Jambo hili husaidia sana katika uimarishaji wa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi. Makala hii ililenga kutimiza malengo mahususi mawili. Lengo la kwanza lilikuwa kujadili dhana ya biashara za kimataifa za kuvuka mpaka na dhana ya uzungumzaji wa Kiswahili na lengo la pili lilikuwa kubainisha mchango wa biashara za kimataifa za kuvuka mpaka katika uimarishaji wa uzungumzaji wa Kiswahili kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini Rwanda. Utafiti uliongozwa na Nadharia ya Utamaduni Jamii. Mbinu za uchanganuzi wa matini na mahojiano zilitumiwa kukusanya data. Usampulishaji lengwa ulitumiwa kupata sampuli ya utafiti kutoka kwenye shule zilizoteuliwa. Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa biashara za kimataifa za kuvuka mpaka zina mchango mkubwa katika uimarishaji wa uzungumzaji wa Kiswahili kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini Rwanda. Isitoshe, utafiti huu umependekeza kuwa walimu wanapaswa kutumia fursa ya biashara za kimataifa za kuvuka mpaka katika uimarishaji wa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi wao.