Ruwaza ya Kiidadi katika Ufafanuzi wa Vidahizo vya Kiantonimu katika Kamusi
Tathmini ya Kamusi Teule
Abstract
Maana za vidahizo katika kamusi huelezwa kwa kutumia mbinu mbalimbali. Miongoni mwa mbinu hizo ni matumizi ya antonimu ambazo hutumika zaidi kufafanua vidahizo vya kamusi za lugha moja kwa sababu walengwa wake huhitaji kupata maana kamilifu zote zinazotafutwa. Kwa msingi huo, antonimu zote zinazohusu kidahizo hutakiwa kuingizwa katika kidahizo husika kwa kufuata utaratibu. Ujitokezaji wa antonimu katika kamusi sio wa kiholela bali huzingatia uhusiano wa kimaana kati ya kidahizo na antonimu husika. Uhusiano huo ndio huamua idadi na aina ya antonimu zinazopaswa kuambatana na kidahizo, hivyo, kuunda ruwaza fulani ambazo huitwa ruwaza za kiidadi. Kuwapo kwa ruwaza hizo kumechangia kufanyika kwa utafiti huu unaotathmini kujitokeza kwa ruwaza za kiidadi katika ufafanuzi wa kiantonimu wa vidahizo vya kamusi wahidiya za Kiswahili. Nadharia Jumuishi ya Leksikografia imetumiwa katika uchambuzi wa data za makala hii. Data za zilikusanywa kutoka katika Kamusi Kuu ya Kiswahili toleo la tatu (yaani KKK3) kwa kutumia mbinu ya uchambuzi wa matini. Jumla ya vidahizo 379 vimebainika kutumia antonimu katika ufafanuzi wake na kuunda ruwaza tano za kiidadi zinazohusu umoja, uwili, utatu, unne na utano kutegemea idadi ya antonimu zilizotumika kuvifafanua vidahizo husika.