Uchambuzi wa Mashartizuizi katika Muundo wa Silabi za Kichasu
Abstract
Makala hii imechunguza muundo wa silabi za lugha ya Kichasu kwa kuzingatia uchambuzi wa mashartizuizi ya Kichasu. Lengo la makala hii ni kubainisha miundo ya silabi za lugha hiyo. Utofauti wa udhihirikaji wa miundo ya silabi katika lugha mbalimbali za Kibantu ndio umechagiza kufanyika kwa utafiti huu. Kutokana na tafiti mbalimbali, kila lugha huwa na mpangilio tofauti wa mashartizuizi na ujitokezaji wa miundo yake huweka mipaka katika miundo ya silabi zake katika maneno. Data zilikusanywa kwa kutumia upitiaji maandiko pamoja na masimulizi kutoka kwa watoataarifa. Data zilichanganuliwa kwa mkabala wa kitaamuli ambapo mbinu ya uchanganuzi kimada imetumika. Uchanganuzi wa data uliongozwa na misingi ya Nadharia ya Umbo Upeo (1993). Matokeo yanaonesha kwamba Kichasu kina jumla ya miundo kumi na mmoja ya silabi inayokubalika kisarufi. Miundo hiyo ni ya silabi nyepesi na ya silabi nzito.