Mitanziko ya Wahusika katika Riwaya Teule za Euphrase Kezilahabi
Abstract
Watunzi wa kazi mbalimbali za fasihi huumba wahusika kwa ustadi mkubwa kwa lengo la kubeba maudhui na kuyafikisha kwa hadhira husika. Wahusika hao hubebeshwa fikra na tafakuri zinazoonesha hisia za mwandishi zinazoambatana na hali fulani katika kutoa maamuzi ya tafakuri yake. Miongoni mwa mambo hayo ni mitanziko ambayo hubainika kupitia matendo wafanyayo wahusika hao. Mitanziko hiyo husababisha wahusika kuchukua maamuzi ya kufanya au kutokufanya jambo fulani. Hivyo, makala hii inabainisha sababu za mitanziko ya wahusika katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi ambazo ni Rosa Mistika (1971) na Kichwamaji (1974). Shabaha ya kubainisha sababu hizo kwa mwegamo wa kifasihi ni kuthibitisha kwamba fasihi ni zao la jamii na kwamba mitanziko inayowakumba wahusika katika riwaya hizo, ni usawiri wa wahusika halisi katika jamii, wanaokumbwa na mitanziko ya namna hiyo katika maisha yao ya kila siku. Data za utafiti huu zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya usomaji matini. Misingi miwili ya Nadharia ya Udhanaishi ilitumika katika uchunguzi, uchanganuzi na uwasilishaji wa matokeo ya makala hii. Matokeo yanaonesha kwamba mitanziko inayowakumba wahusika katika riwaya teule inatokana na sababu kuu tatu, ambazo ni: za kijamii, kiutamaduni na kifalsafa.