Michakato ya Kisintaksia ya Uundaji wa Sentensi Changamani za Kiswahili
Abstract
Makala hii inalenga kuchambua michakato ya kisintaksia ya uundaji wa sentensi changamani za Kiswahili kwa kubainisha namna kishazi kikuu na kishazi bebwa vinavyowekwa pamoja kuunda sentensi hizo. Ili kufanikisha lengo hilo, makala imeongozwa na Nadharia Rasmi ya Chomsky (1965). Data za makala hii ni sentensi changamani za Kiswahili ambazo zilikusanywa kwa njia ya usomaji wa matini kutoka katika riwaya na magazeti. Matini hizi ziliteuliwa kwa kutumia mbinu ya usampulishaji nasibu sahili. Uchambuzi wa data ulifanyika kwa mkabala wa kitaamuli kwa kutumia mbinu ya uchambuzi wa kimaudhui. Makala hii imebaini kwamba kuna michakato mitatu inayotumika kuunda sentensi changamani ambayo ni uchopekaji, udondoshaji-chopezi na udondoshaji-chopezi hamishi. Kwa kutumia Nadharia Rasmi, imebainika kwamba kila mchakato una hatua zake katika kuunda sentensi changamani.