Itikadi katika Riwaya za Awali za S.A Mohamed
Abstract
Wahakiki wengi wanapozungumzia msimamo na mielekeo ya mwandishi kuhusu maisha na ulimwengu uliomzunguka, huchukulia kwamba msimamo huu ni mmoja na tengemano. Ni kama kwamba mtunzi huongozwa na itikadi moja ambayo ni imani yake inayosawiri mtazamo wake kuhusu jamii katika kazi yake. Makala hii inanuia kuonyesha kuwa itikadi ni dhana badilifu na nyumbufu kulingana na namna mtunzi anavyowasilisha kazi yake, masuala makuu anayojadili, anavyosawiri wahusika wake, na mtindo mzima wa kazi yake. Itikadi ndiyo huelekeza misimamo, mielekeo na imani ya mtunzi na hivyo kuathiri mtazamo wa mwandishi kuhusu ulimwengu unaomzunguka ambao huweza kubadilika. Ni katika mkabala huu ambapo makala hii inalenga kutathmini namna itikadi katika riwaya za awali za S.A Mohamed ambazo zinawakilishwa na Asali Chungu (1978) na Kiza katika Nuru (1986) zinavyojitokeza ili kudhihirisha itikadi na dhana badilifu na nyumbufu na hivyo msimamo wa mtunzi huwa changamano wala sio mmoja na tengemano kama inavyofikiriwa na wahakiki wengi wa fasihi. Aidha, tutaonyesha kuwa itikadi ina mielekeo tofauti kwani itikadi ya mtunzi na itikadi tawala huweza kuwa tofauti.