' Iktibasi ' katika Tenzi za Mwanakupona na Al-Inkishafi

Authors

  • Beja S Karisa University of Dar es Salaam
  • Abdulrahman Mwinyifaki

Abstract

Makala haya yanatazama tenzi za kale za Kiswahili kwa mkabala wa kitabu kitukufu cha Kurani na Sunnah za Mtume Muhammad (SAW). Wahakiki wengi wamechambua tenzi hizi za kale na kutoa maoni kwamba zina maudhui ya dini ya Kiislamu. Hata hivyo ushahidi halisi wa jinsi watunzi walivyochota maudhui yao kutoka kwenye Kurani Tukufu na Sunnah1 haujawekwa bayana na utafiti wowote. Makala haya yamelenga kuziba mwanya huu kwa kuonesha jinsi watunzi wa tenzi za Mwanakupona na Al-Inkishafi walivyochota kutoka kwenye Kurani Tukufu na Sunnah kifungu baada ya kifungu na kujenga maudhui yao ya dini ya Kiislamu katika fasihi bila wao kusema kazi zao zinatokana na Kurani Tukufu na Sunnah. Mfumo huu wa kutumia Kurani Tukufu na Sunnah bila kubainisha kuwa ni Kurani Tukufu au Sunnah kwa lugha ya Kiarabu huitwa "Iktibasi". Makala haya yameongozwa na nadharia ya Uislamu. Taib (2004) ameeleza kwa kirefu nadharia hii kwamba imejikita katika nguzo tano za Uislamu. Lengo kuu ni kuonyesha jinsi watunzi wanavyoweza kuhuisha vifungu vya Kurani Tukufu na Sunnah katika miktadha halisi kwa njia ya kubuni na kuvitumia kama misingi ya mahubiri ya mtu binafsi na kwa umma. Katika makala haya tunaona kwa yakini uhusiano uliopo kati ya dini ya Kiislamu na fasihi. Dini inanufaishwa na fasihi kupitia mahubiri yenye msingi wa kifasihi nayo fasihi inasambazwa kupitia mahubiri ya kidini. Mbali na kudhihirisha uhusiano wa dini na fasihi makala haya ya uchanganuzi wa tenzi hizi ni muhimu kwa maulamaa na waandishi wa fasihi kwa kuona jinsi wanavyoweza kuchota vifungu teule vya Kurani Tukufu na Sunnah kama msingi wa mahubiri kwa wanajamii kwa njia za kifasihi.

1 Sunnah haitoki moja kwa moja katika Kurani; inatokana (i) Failiyyu - matendo aliyofanya Mtume Mohammad (S.A.W), (ii) Qauliyyu - maneno aliyosema Mtume Muhammad (S.A.W) kwa wafuasi wake na (iii) Takririyyu €“ kimya alichotumia Mtume Muhammad (S.A.W) kuashiria kukubalika kwa jambo ambapo kama jambo halikuwa zuri Mtume angalisema kuwa si zuri.

Downloads

Published

2017-08-22

Issue

Section

Articles