Uchunguzi wa Mbinu na Vifaa vya Kufundishia Utamaduni wa Lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Burundi
Abstract
Makala hii imelenga kuchunguza mbinu na vifaa mbalimbali vinavyotumiwa na walimu kufundishia utamaduni wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Burundi. Katika ukusanyaji wa data, hojaji na ushuhudiaji ndizo mbinu zilizotumiwa. Nadharia ya Utamaduni-Jamii ya Vygostsky (1980) ilitumika katika uchanganuzi wa data. Data ilichambuliwa kwa kutumia majedwali, maelezo na programu tumizi ya kuchambua data ya SPSS (Statistical Package for the Social Sciences). Matokeo yameonesha kuwa baadhi ya walimu wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Burundi wanaingiza masuala ya utamaduni katika ufundishaji na wanatumia mbinu tano katika ufundishaji wao. Hata hivyo, matokeo yameonesha kwamba mbinu mbili ambazo ni uigizaji na majadiliano kuhusu vitabu na matini za Kiswahili ndizo zinazotumiwa kwa kiwango kikubwa. Kuhusu vifaa vya kufundishia masuala ya utamaduni wa Kiswahili, utafiti huu umedhihirisha kuwa vitabu, intaneti, projekta na kompyuta ndivyo vifaa vinavyotumiwa kwa asilimia kubwa. Walimu wameshauriwa kubuni mbinu na vifaa vinavyoweza kuwasaidia kufanikisha mafunzo ya utamaduni wa Kiswahili kwa sababu lugha na utamaduni havitenganishwi.