Mazingira ya Utokeaji wa Alomofu za Utendeshi katika Lugha ya Kimalila

Authors

  • Azimio Sote Mhadhiri

Abstract

Makala hii inachambua alomofu za utendeshi zinazojitokeza katika vitenzi vya lugha ya Kimalila lengo likiwa kuchambua mazingira ya kutokea kwa alomofu za utendeshi zilizopo na chanzo cha kutokea kwake. Mbinu za uchanganuzi wa matini na hojaji zilitumika kukusanyia data zilizotumika katika utafiti huu. Aidha, Nadharia ya Umboupeo iliongoza utafiti huu. Matokeo yanaonesha kwamba alomofu za utendeshi katika lugha ya Kimalila zipo zinazotokea katika mazingira yanayotabirika na nyingine yasiyotabirika. Lugha ya Kimalila ina alomofu za utendeshi fupi na ndefu. Alomofu fupi ni {-y-} na {-w-} na alomofu ndefu ni {-isy-}, {-izy-}, {-iz-}, {-iziz-},  {-ishiz-}, {-isiz-}, {-wiz-} na {-ikh-}. Alomofu hizi hutokea kutegemeana na kanuni za tangamano la irabu kama ilivyo kwa lugha nyingi za Kibantu. Sifa za mzizi na mfuatano wa utendeshi na utendea zinachochea kwa kiwango kikubwa kutokea kwa alomofu hizi za utendeshi. Mazingira ya kutokea kwa alomofu za utendeshi {-w-}, {-wiz-} na {-iziz-} yanaonesha upekee katika utokeaji wake. Makala inahitimisha kuwa kuna mazingira ya uteuzi na matumizi ya alomofu za utendeshi yanayofungwa na lugha mahususi (Kimalila), jambo linalofungua milango kwa tafiti zaidi katika lugha nyingine kiulinganisho.

DOI: https://dx.doi.org/10.4314/kcl.v23i1.2

 

Author Biography

Azimio Sote, Mhadhiri

Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mbeya, Tanzania

Downloads

Published

2025-06-30