Jiografia ya Binadamu kama Mtaimbo Endeshi wa Anthroposenia katika Riwaya za Bustani ya Edeni, Vipuli vya Figo, Mafuta na Walenisi
Abstract
Makala hii inashughulikia jiografia ya binadamu kama mtaimbo endeshi wa anthroposenia katika riwaya za Emmanuel Mbogo: Bustani ya Edeni, Vipuli vya Figo; na za Katama Mkangi: Mafuta na Walenisi. Riwaya hizi nne zilisomwa kisha data zilitongolewa mintarafu ya kusudi la makala hii. Suala la anthroposenia lilichanganuliwa katika misingi ya kipindi ambacho taathira yake ingalipo na inaendelea kuwanda kiwakati katika maisha ya binadamu. Lengo kuu la makala hii ni kujadili namna janibu mbalimbali anazoishi na kuzitawala mwanadamu zilivyo na jukumu la kuhimili uendeshaji wa anthroposenia mbele, hususani za Afrika, tofauti na mabara mengine tajiri kama vile Uropa na Marekani. Nadharia ya Uhakikimazingira iliongoza uhakiki wa data za makala hii. Matokeo ya utafiti yanadhihirisha kwamba janibu fukara duniani huimarisha na huwa mtaimbo endeshi wa anthroposenia kuliko zile zenye ukwasi. Waandishi wamefanikiwa kudhihirisha wazi kuwa viongozi wa mataifa tajiri wanaelewa hili na hivyo wanayachafua na kuyaharibu zaidi mazingira ya mataifa fukara kuliko yao wenyewe.