Dhima ya Lugha ya Mhusika Mtoto katika Vichekesho Teule vya Anko Zumo
Abstract
Vichekesho ni kipera cha fasihi simulizi kinachoendelea kukua na kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Hii inamaanisha kuwa kama ambavyo mambo mengi yamebadilika kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, sanaa ya vichekesho nayo imebadilika, hususani katika vipengele vya uhifadhi na uwasilishaji wake. Hivi sasa vichekesho vinawasilishwa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, kama vile YouTube, Instagram, Facebook na Twitter. Anko Zumo ni miongoni mwa vichekesho vinavyowasilishwa kupitia mitandao ya kijamii. Vichekesho hivi hutumia wahusika watu wazima na watoto. Miongoni mwa wahusika wakuu wa vichekesho hivi ni mtoto Maisara Mohamed maarufu kama Mai Zumo. Mhusika huyu anatumia lugha ili kuivutia hadhira na kuifanya icheke. Licha ya kuivutia hadhira na kuifanya icheke, zipo tafiti mbalimbali zinazoonesha kuwa matumizi ya watoto katika kazi za sanaa hayafanyiki kiholela bali huwa na dhima anuwai. Suala hili liliibua makala hii ambayo imelenga kuchunguza dhima ya lugha ya mhusika mtoto katika vichekesho vya Anko Zumo. Data za makala hii zilipatikana kwa kuchunguza vichekesho teule tisa (9) kupitia mtandao wa YouTube. Uchambuzi wa data uliongozwa na Nadharia ya Uvunjaji wa Kanuni Usio na Madhara. Matokeo yanaonesha kuwa lugha ya mhusika mtoto katika vichekesho teule vya Anko Zumo ina dhima anuwai.