Mchakato wa Kutathmini Makala

Kioo cha Lugha ni jarida ambalo makala zake zinatathminiwa walau na wasomaji wawili bila kuonesha mwandishi au mtathmini ni nani. Waandishi wanatakiwa kuepuka kuonesha utambulisho wowote unaowahusu katika makala ili wanaoitathmini wasimfahamu mwandishi. Miswada inayowasilishwa kwa ajili ya kuchapishwa inasomwa na walau wasomaji wawili ambao ni mahiri na wataalamu wa mada husika. Makala inapowasilishwa inapitiwa kwanza na Mhariri Mkuu wa jarida ili kuhakikisha kwamba imetimiza mahitaji ya jarida kabla haijatumwa kwa watathmini wa nje kutoka katika kanzidata yetu. Kama maudhui ya makala yanakidhi mawanda na sera za jarida, mhariri atatuma makala kwa watathmini wawili ambao hawajulikani na mwandishi, kuwaomba kukubali kuitathmini makala. Watathmini wataitathmini miswada wakilenga kuangalia ubora wake katika maudhui, uwazi wa uwasilishaji, uasili, mchango wake kitaaluma na uzito wake kimaudhui na kiutafiti. Muda wa kukamilisha zoezi hili unategemea na kupatikana kwa watathmini. Hata hivyo, kwa kawaida, inachukua wiki nne mpaka nane. Inategemea maoni ya watathmini, mwandishi anaweza kuhitajika kufanya marekebisho madogo au makubwa ya makala yake. Kama atatakiwa kufanya marekebisho makubwa, mwandishi atapaswa kutuma tena makala yake ili ikatathminiwe tena na watathmini. Inatokea wakati mwingine makala kukataliwa kabisa. Baada ya mwandishi kuingiza marekebisho ya makala yake, wahariri wataipitia miswada tena kabla ya kukubaliwa kuchapishwa. Waandishi ambao makala zao zitakubaliwa kuchapishwa, watapatiwa nakala moja ya jarida lenye makala husika.

 

 

 

ISSN 0856-552 X (nakala ngumu) & ISSN 2546-2210 (mtandaoni)