KUFAA KWA NADHARIA YA UCHANGANUZI VIJENZI KATIKA UCHAMBUZI WA HIPONIMIA
Abstract
Hiponimia ni mojawapo ya mahusiano ya kifahiwa inayoashiria uhusiano ambapo leksimu ya jumla inajumuisha kimaana leksimu mahususi. Uhusiano wa leksimu kihiponimia ulidhukuriwa kuwa unafanana katika lugha anuwai ulimwenguni na aghalabu unahusisha leksimu nomino pekee. Hata hivyo, tafiti za hivi punde zinadhihirisha kuwa hiponimia huonekana pia miongoni mwa vivumishi, vielezi na vitenzi na huweza kutofautiana kimuundo na kimtindo kutoka lugha moja hadi nyingine kwa sababu ya tofauti za kitamaduni. Wataalamu anuwai wamekuwa na mapendekezo kadha kuhusu nadharia ifaayo ya kuainisha leksimu za lugha kihiponimia. Wengine wanaelekea kupendelea matumizi ya nadharia ya Kiini Maana (Core Meanings Theory) na Nadharia ya Sampuli Kifani (Prototype Theory). Hata hivyo inadhihirika kuwa nadharia ya Uchanganuzi Vijenzi (Componential Analysis) inafaa zaidi katika uchanganuzi wa hiponimia ya leksimu nomino, vitenzi, vivumishi na vielezi. Makala haya yanaangazia kufaa kwa nadharia hii katika uhakiki wa hiponimia ikilinganishwa na nadharia Kiini Maana na Sampuli Kifani.