Uhusiano wa Kimatengo na Kindendeule: Ushahidi wa Kiisimu

Gervas A. Kawonga, Mussa M. Hans

Abstract


Kumekuwa na mijadala ya wanazuoni mbalimbali kuhusu uhusiano uliopo baina ya Kimatengo na Kindendeule. Lengo la makala haya ni kuweka wazi madai ya uhusiano uliopo baina ya lugha hizi mbili. Lugha hizo zinazodaiwa kufanana zinatengana kijiografia kwa umbali wa zaidi ya kilometa 200. Aidha, utengano huo unaongezwa na kuwepo kwa jamiilugha ya Wangoni katikati ya lugha hizo. Lugha ya Kingoni haielekeani kiisimu na lugha hizo mbili. Licha ya utengano huo, kuna madai ya muda mrefu kwamba Kimatengo na Kindendeule ni lugha zinazofanana. Makala haya yalitumia data ya uwandani ili kupata ushahidi wa kiisimu unaoweza kueleza kiwango cha kufanana au kutofautiana baina ya lugha hizo mbili. Mbinu za hojaji na majadiliano zilitumika kupata msamiati wa msingi na sauti ili kupata fonimu za lugha hizo. Data ya utafiti ilijikita kwenye kigezo cha msamiati wa msingi na kigezo cha kifonolojia. Kwa kutumia Takwimuleksika kama kiunzi cha uchambuzi, matokeo ya vigezo vyote viwili yanaonesha kwamba lugha hizo zinafanana kwa wastani wa asilimia 87.7, kiwango ambacho kinazifanya kuwa kwenye uhusiano wa kilahaja. Lahaja katika makala haya ni dhana inayotumika kueleza kiwango cha juu cha kufanana kwa lugha mbili au zaidi. Kwa mtazamo wa fasili hii, watu wote wanazungumza lugha, dhana ya lahaja inatumika kueleza uhusiano wa kiwango cha juu cha uhusiano wa lugha mbili au zaidi. Hitimisho la makala haya ni kwamba vigezo viwili vilivyotumika ni kuntu na ni ithibati ya kudai kwamba Kimatengo na Kindendeule ni lugha zenye uhusiano wa kilahaja.


Full Text:

PDF

Refbacks

  • There are currently no refbacks.