Tathmini ya Mchakato wa Utenzishaji katika Kiswahili na Hadhi ya Msamiati wake Kikamusi
Abstract
Tofauti na unominishaji, dhana ambayo imezoeleka sana katika taaluma za Kiswahili kama mchakato wa kimofolojia wa kubadili kategoria nyingine za maneno kuwa nomino, utenzishaji ni dhani ngeni. Utenzishaji pia ni mchakato wa kimofolojia wenye kuzalisha vitenzi kutokana na kategoria za maneno. Uzalishaji wa vitenzi kutokana na kategoria nyingine za maneno ni mchakato ambao haujachunguzwa sana katika Kiswahili ukilinganisha na mchakato kama wa unominishaji. Uimarishaji na utanuzi wa lugha kimsamiati unaweza pia kufanywa kwa mbinu kama hizi ili kusaidia lugha (Kiswahili) kupata istilahi toshelevu za kiufundi na kisanyansi ili kukidhi mapinduzi ya kisayansi na kiteknolojia ambayo yanaenda kwa kasi katika nyanja mbalimbali. Kwa hiyo, makala haya ya inatathmini uwezo wa kategoria za maneno mbalimbali ya Kiswahili katika kuzalisha vitenzi na yanatathmini hadhi ya vitenzi hivyo, kimofolojia, kisemantiki na kikamusi. Aidha, makala haya yanabainisha viambishi tenzishi na kutathmini uzalifu wake ili kuweka bayana uwezo wa utenzishaji kimsamiati katika Kiswahili.