Mambo yanayochangia Mvutano kati ya Maarifa ya Kiujaala na Maarifa ya Kiujarabati katika Maudhui ya Filamu za Kiswahili
Authors
Asnath Charles
University of Dar es salaam
Abstract
Maarifa yanaelezwa kuwa katika vyanzo vingi vikiwamo kutoka katika milango ya fahamu au hisi (common sense knowledge), maarifa ya kisayansi, maarifa ya kifalsafa na maarifa ya kiujaala, yaani imani katika miungu. Uchunguzi huu umetumia istilahi ujarabati kurejelea maarifa ya aina tatu za mwanzo. Lengo kuu la makala hii ni kueleza mambo yanayochangia kuzuka kwa mvutano kati ya maarifa ya kiujaala na maarifa ya kiujarabati katika dhamira za filamu za Kiswahili katika kipindi cha sasa. Data zilikusanywa kutoka maktabani na uwandani katika mkoa wa Dar es Salaam na Arusha. Nadharia ya Mwitiko wa Msomaji ilitumika na mbinu ya utazamaji wa sidii, hojaji na usaili zilitumika kukusanya data. Utafiti huu ulitumia mkabala wa kitaamuli na mkabala wa kitakwimu. Idadi ya filamu teule zilikuwa nane, mbili kwa kila mtunzi. Filamu teule zilizotumika ni pamoja na God`s Kingdom na Revelation za Emmanuel Myamba, Mkwe na Big Surprise za Lea Richard, White Maria na Point of No Return za Mtitu Gabriel na Jini Sonia na Radi Kobra za July Tax. Makala hii inaripoti kuwa yapo mambo mengi yanayochangia kuwapo kwa mvutano kati ya ujaala na ujarabati unaooneshwa katika filamu za Kiswahili Tanzania. Mambo hayo ni pamoja na uhalisia wa jamii, changamoto za kiutafiti, mabadiliko katika tasnia ya filamu, kutojitosheleza kwa ujaala na ujarabati pamoja na kutofautiana kwa viwango vya elimu.