Mkabala wa Kimawasiliano katika Ufundishaji wa Lugha ya Pili: Mifano kutoka Ufundishaji wa Kiswahili kwa Wageni Tanzani
Authors
Kijakazi Omar Makame
University of Dar es salaam
Abstract
Wataalamu wa isimu tumizi wanakubaliana kuwa mkabala wa kimawasiliano ni faafu zaidi ukilinganishwa na mikabala ya kijadi katika ufundishaji wa lugha. Mikabala hiyo ya kijadi ni pamoja na sarufi-tafsiri na usikilizaji (Nunan, 2004). Mikabala hiyo ilijikita katika kuangalia ufundishaji wa lugha kuwa ni mchakato wa kujenga tabia ambazo zilipatikana kwa wanafunzi kurudia na kukariri miundo ya sarufi bila ya kuangalia umuhimu wa mawasiliano katika lugha wanayojifunza. Makala hii inalenga kuufafanua mkabala wa kimawasiliano katika ufundishaji wa lugha ya pili kwa kutumia mifano kutoka ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni. Sababu hasa ya kufafanua mkabala huu ni kwamba walimu wengi wanaonekana kuutumia mkabala huu lakini si kwa kiwango kinachohitajika. Hivyo basi, makala hii itajaribu kufafanua vipengele na kanuni mbalimbali za mkabala huu ili kuweza kuzibainisha na kuzitolea mifano kupitia ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni. Data za utafiti huu zimekusanywa uwandani ambapo zimehusisha walimu kumi na mmoja kutoka katika vituo vinne tofauti vya ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni nchini Tanzania. Data zimechambuliwa kwa kutumia mkabala wa kimaelezo na imebainika kwamba walimu wengi hawautumii vizuri mkabala wa kimawasiliano. Hivyo, imependekezwa kwamba mafunzo yanayotolewa kwa walimu kuhusu mkabala huu yafafanue vizuri kuhusu kanuni na mbinu mbalimbali za mkabala huu ili kuwawezesha walimu kuutumia ipasavyo na kuwawezesha wanafunzi kufikia ufasaha na usahihi katika ujifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya pili au ya kigeni.