Mwelekeo Mseto: Utekelezwaji wake kwenye Vitabu vya Kiada na katika Ufundishwaji wa Kiswahili Sekondari; Kaunti ya Machakos, Kenya
Authors
Ombito Elizabeth Khalili
University of Kenyatta
Abstract
Utafiti huu ulihusu utekelezwaji wa mwelekeo mseto katika ufundishaji wa Kiswahili kwa kutumia vitabu vya kiada vilivyoidhinishwa katika shule za sekondari, nchini Kenya. Utafiti huu ulilenga kutathmini ufahamu na maoni ya waandishi wa vitabu na wanajopo wa jopo la Kiswahili la ngazi ya sekondari kuhusu utekelezwaji wa mwelekeo mseto vitabuni; kukadiria viwango vya usetaji wa mada kwenye vitabu vya kiada vilivyoidhinishwa; na kuchunguza utekelezwaji wa mwelekeo mseto kwa ufundishaji wa Kiswahili uliofanywa na walimu walipofunza Kiswahili darasani katika shule za sekondari. Nadharia iliyoelekeza utafiti ni Ruwaza ya Usetaji wa Lugha iliyoasisiwa na Enreight na McCloskey (1988). Utafiti huu ulitumia mbinu ya utafiti elezi yenye mtazamo wa kibunilizi. Sampuli ya utafiti ilijumuisha vitabu vya kaida 23 vilivyoidhishwa kufunzia Kiswahili sekondari; waandishi 28 wa vitabu vya kiada; wanajopo sita wa jopo la Kiswahili sekondari waliohudumu katika Taasisi ya Wakuza Mitaala ya Kenya (TYWM), na walimu 60 waliofunza Kiswahili kwa wanafunzi wa kidato cha tatu Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa: waandishi wa vitabu vya kiada walikuwa na ufahamu wa kutunga miswada kwa mwelekeo mseto ingawa hawakulazimika kutekeleza mwelekeo mseto vitabuni kwa vile haukuzingatiwa kwenye uteuzi wa miswada ya vitabu vya kiada na TYWM.