Usahilishaji wa Irabuunganifu za Kiingereza katika Kiswahili Sanifu
Abstract
Mwingiliano wa lugha ya Kiingereza na lugha ya Kiswahili umesababisha utohoaji wa maneno ya Kiingereza katika lugha ya Kiswahili. Maneno yenye irabuunganifu ni mojawapo ya maneno yanayotoholewa katika lugha ya Kiswahili. Kutokana na hilo, baadhi ya wanaisimu wanadai kuwa katika lugha ya Kiswahili kuna irabuunganifu kama matokeo ya utohoaji wa maneno ya lugha ya Kiingereza. Hata hivyo, makala haya yanapinga mtazamo huo kwa kuonesha kuwa irabuunganifu zinapoingizwa katika lugha ya Kiswahili husahilishwa kuwa irabu za Kiswahili. Data ya makala haya imekusanywa kutoka Kamusi ya Kiingereza-Kiswahili (TUKI, 2006) na uchambuzi wa data umeongozwa na Nadharia ya KI ya Clements na Keyser (1983) inayohusu uwalikilishi wa silabi katika neno. Matokeo ya makala haya yanaonesha kuwa irabuunganifu za Kiingereza husahilishwa ili kupata irabu sahihi za Kiswahili sanifu. Vilevile, imebainika kuwa irabuunganifu zinazoshindikana kusahilishwa huvunjwavunjwa na moja (hasa ya kulia) huunda silabi yake yenye muundo wa irabu pekee. Kwa hiyo, irabuunganifu za Kiingereza [eɪ, eɪ, aɪ, aʊ, əʊ] husahilishwa kuwa irabu za Kiswahili [a, ɛ, i, ɔ, ɔ] mtawalia. Kimsingi, usahilishaji huu huzingatia matamshi ya lugha ya Kiingereza kwa namna yanavyosikika kwa wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili. Hivyo basi, makala haya yanaunga mkono kutokuwapo kwa irabuunganifu katika lugha ya Kiswahili. Kwa maana hiyo, lugha ya Kiswahili ina irabu tano [a, ɛ, i, ɔ, na u] ambazo huweza kutokea kama irabundefu katika mazingira tofautitofauti.