Uchanganuzi wa Vimaanilizi vya Maana ya Misemo ya Vyombo vya Usafiri katika Jiji la Dodoma
Abstract
Makala haya inajikita katika uchanganuzi wa vimaanilizi vya maana ya misemo ya vyombo vya usafiri. Data za utafiti huu zilikusanywa kwa njia ya ushuhudiaji, usaili na majadiliano katika kundi. Jumla ya misemo 110 ilikusanywa kwa kunukuu misemo husika kutoka katika vyombo vya usafiri katika Jiji la Dodoma. Washiriki 10 walishirikishwa katika utafiti huu; nao walikuwa ni madereva na mautingo. Mtafiti alitumia mbinu ya bahati nasibu ili kupata washiriki. Washiriki walifuatwa kwenye maegesho ya magari. Misemo iliyokusanywa ilichunguzwa ili kuona kama inakidhi lengo la utafiti huu. Baadhi ya misemo ambayo haikufaa iliondolewa na iliyofaa ilichanganuliwa maana zake kwa misingi ya kipragmatiki hasa kipengele cha vimaanilizi vya maana. Matokeo ya utafiti huu yameonesha kuwa misemo inayoandikwa katika vyombo tajwa husheheni maana mbalimbali ambazo waandishi hawaziweki wazi. Kwa kuzingatia muktadha wa mawasiliano husika, makala haya yamepambanua maana hizo. Pia, inapendekezwa kuwa utafiti zaidi ufanyike kwa kutumia kiunzi cha kipragmatiki katika matini andishi. Makala yanahitimisha kuwa maana msingi na maana za ziada hutegemeana na hukamilishana katika kutimiza lengo la mawasiliano.