Taathira ya Maisha ya Msanii, Jamii na Wakati katika Kazi ya Fasihi: Ulinganishi wa Tenzi za Wasia
Abstract
Kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala miongoni mwa wanafasihi kuhusu uchambuzi wa kazi za fasihi. Kuna wanaodai kuwa kazi za fasihi zinapaswa kuchambuliwa bila kuhusishwa na kitu kingine nje ya kazi hizo. Vilevile, kuna wanaodai kuwa mfungamano wa fasihi na jamii ni suala dhahiri, na kwa namna yoyote ile, haiwezekani kuitenga jamii na kazi husika ya fasihi. Hivyo, makala haya yanatoa mchango katika hoja kuwa uchambuzi wowote wa kifasihi ni muhimu ukamzingatia msanii wa kazi husika, jamii yake na wakati alioishi. Makala yanatumia Nadharia ya Mwigo kuonesha jinsi maisha ya wasanii, jamii zao na wakati walioishi vilivyo na taathira katika tenzi za wasia za Mwana Kupona, Hati na Adili pamoja na Mwanangu Nakuusia. Mahitimisho ya makala haya yanatokana na data zilizokusanywa kwa kutumia uchambuzi matini, usaili, majadiliano na dodoso na kuchambuliwa kwa kutumia mkabala wa kitaamuli.