Dhima ya Ontolojia ya Kiafrika katika Jaala ya Shujaa wa Utendi wa Rukiza
Abstract
Makala haya yanahusu uchunguzi wa dhima ya Ontolojia ya Kiafrika katika jaala ya shujaa wa utendi wa Rukiza. Utafiti huu ni wa maktabani na uwandani. Mbinu zilizotumika kukusanya data ni uchanganuzi wa matini na mahojiano. Lengo la makala haya ni kuonesha kuwa licha ya kuwapo kwa mwingiliano wa kiontolojia katika jamii, ontolojia ya Kiafrika ina dhima katika tendi za Kiafrika. Kwa kutambua hilo, makala yamefafanua dhima ya ontolojia ya Kiafrika katika utendi wa Rukiza. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kwamba dhima ya vipengele vya ontolojia ya Kiafrika ni kudhihirisha jaala ya shujaa, kumpatia shujaa nguvu za kimwili na nguvu za sihiri, kumpatia shujaa msaada wa mizimu unaomwezesha kuondoa vikwazo vinavyomkabili, kumlinda shujaa asidhurike, kumpatia shujaa silaha bora zenye nguvu za sihiri na kumwezesha shujaa kutatua changamoto za jamii yake. Kwa ujumla, makala haya yanahitimisha kuwa vipengele vya ontolojia ya Kiafrika vina dhima kubwa katika jaala ya shujaa wa utendi wa Rukiza. Shujaa akifungamana vyema na vipengele vya ontolojia ya Kiafrika, hutimiza jaala yake. Kwa upande mwingine, shujaa akivunja mshikamano huo hubadili jaala yake.