Umuhimu wa Mtindo wa Uhalisiajabu katika Riwaya ya Babu Alipofufuka (2001)
Abstract
Mijadala kuhusu mtindo wa uhalisiajabu imetawala sana miongoni mwa wataalamu wa fasihi. Baadhi yao ni Strecher (1999) ambaye ameangalia namna mtindo huo unavyowakilisha uhalisi wa maisha. Khamis (2007b) na Madumulla (2009) wamebainisha umuhimu wa mtindo huu kwa kuuhusianisha na suala la ubunifu wa mtunzi, ambapo wamejikita zaidi katika muktadha wa kifani. Kwa kuzingatia mawanda ya tafiti mbalimbali zilizokwishafanywa, makala haya yamekusudiwa kupanua mawanda ya kiutafiti na kubainisha kwa kina umuhimu wa mtindo huo kwa kujiegemeza katika muktadha wa kiujumi, kiepistemolojia na kijamii, huku mifano ikitolewa kutoka riwaya ya Babu Alipofufuka ya Said Ahmed Mohammed. Data za utafiti zilipatikana maktabani kwa kutumia mbinu ya usomaji matini. Mjadala uliongozwa na nadharia mbili. Nadharia ya kwanza ni Uhalisiajabu, ambayo ilimwezesha mtafiti kubaini matukio mbalimbali ya kihalisiajabu ndani ya riwaya hiyo. Nadharia ya pili ni Uhemenitiki, ambayo ilimwongoza mtafiti kubaini maana zinazojitokeza ndani ya riwaya hiyo. Matokeo ya utafiti yamebainisha kuwa mtindo wa uhalisiajabu una umuhimu mkubwa kiujumi, kiepistemolojia na kijamii.