Uhalisia wa Viambishi vya Kibantu: Uchunguzi wa Viambishi vya Kauli katika Vitenzi vya Kiswahili vyenye Asili ya Kiarabu
Abstract
Lengo la makala haya ni kuonesha uhalisia wa viambishi vya Kibantu kwa kuchunguza viambishi vya kauli za vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu. Data iliyotumika katika makala haya imepatikana kutokana na mbinu ya upitiaji wa nyaraka na usaili. Nyaraka hizo ni Kamusi Kuu ya Kiswahili ya BAKITA na Longhorn (2015) na riwaya za Duniani Kuna Watu ya Abdulla (1973) na Kuli ya Shafi (1979). Vilevile, mbinu ya usaili ilitumika kupata data kutoka kwa wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili wenye uwezo wa kuyatambua maneno ya Kiswahili yenye asili ya Kiarabu. Kutokana na mbinu hizo vimepatikana vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu. Vitenzi hivyo vinapokea viambishi mbalimbali vyenye asili ya Kibantu. Upokeaji wa viambishi hivyo una namna unavyovifananisha na kuvitofautisha vitenzi hivyo na vitenzi vya Kiswahili asilia pamoja na vitenzi vya Kibantu kwa ujumla. Ubainishaji wa viambishi hivyo umezingatia viambishi vya ruwaza ya vitenzi vya Kibantu. Kutokana na ruwaza hiyo, umeoneshwa uhalisia wa viambishi vya kauli za vitenzi (KAV) katika vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu. Pia, kutokana na ruwaza hiyo na uchanganuzi wa data kwa kutumia Nadharia ya Mofolojia Leksika, imebainika kuwa vipo viambishi vya KAV vinavyojitokeza na visivyojitokeza katika vitenzi hivyo, na vyenye ughairi.