Ushairi wa Simu Tamba wa Waswahili wa Pwani ya Kenya
Abstract
Katika makala hii tunajadili jinsi simu tamba inavyotumika kama nyenzo katika uandishi, ukuzaji na usambazaji wa ushairi miongoni mwa Waswahili wa Pwani ya Kenya na hatimaye watu wengine kote ulimwenguni. Ili kutimiza malengo haya tumetumia dhana ya utandawazi kama dhana changanuzi na vilevile Nadharia ya Kisosholojia ya Kiuhakiki lli kuchambua masuala ya kimaudhui ya ushairi wa simu tamba. Data ya utafiti huu imekusanywa kutokana na kutangamana na jumuiya ya Waswahili wa Pwani ya Kenya kupitia simu tamba. Mmoja wa waandishi wa kazi hii pia ni Mswahili wa Pwani ya Kenya na mshiriki katika mitagusano hii ya ushairi wa simu tamba. Katika kazi hii tumeangazia maudhui ya ushairi wa simu tamba miongoni mwa Waswahili wa Pwani ya Kenya na vilevile kuonesha baadhi ya mitindo inayopendelewa katika ushairi huu. Imebainika kuwa maudhui ya ushairi wa simu tamba katika eneo la Pwani ya Kenya yanahusu salamu za kutakiana heri siku ya Ijumaa na wakati wa mfungo wa Ramadhani. Masuala mengine ya kijamii yanayojitokeza ni yale yanayofungamana na ndoa, dini, uchumi na siasa. Imedhihirika pia kuwa mashairi ya simu tamba yanatungwa kwa kuzingatia kanuni za kijadi kama vile kuwa na urari wa vina, kupangilia shairi kwa kutumia beti, kuwa na mishororo iliyokadiriwa, na kuwa na urari wa vina na mizani. Mengi ya mashairi ya Waswahili wa Pwani ya Kenya ni ya muundo wa tathlitha na tarbia. Hata hivyo, kuna changamoto za kutunga na kuuendeleza ushairi wa Kiswahili kwa njia ya simu tamba kama vile ugumu wa kupangilia mishororo na hata vipande vya mashairi kwa namna inayofungamana na arudhi.