Uhawilishaji wa Lafudhi ya Kihehe na Athari zake katika Mawasiliano ya Wajifunzaji wa Kiswahili Sanifu kama Lugha ya Pili
Abstract
Makala hii inachunguza uhawilishaji wa lafudhi ya Kihehe na athari zake katika mawasiliano ya wajifunzaji wa Kiswahili sanifu kama lugha ya pili (L2). Sababu iliyochochea kufanyika kwa utafiti huu ni kuwa uhawilishwaji wa lafudhi ya Kihehe umebainika kupotosha maana na kukwamisha mawasiliano miongoni mwa wajifunzaji lugha ya Kiswahili sanifu wa jamii ya Wahehe. Data za makala hii zilikusanywa kutoka kwa wajifunzaji wa lugha ya Kiswahili sanifu wa jamii ya Wahehe ambao Kihehe ni lugha mama yao. Data za msingi za makala hii zilikusanywa kwa mbinu za masimulizi ya hadithi na uchambuzi wa nyaraka. Uchambuzi wa data uliongozwa kwa Nadharia za Usasanyuzi Linganishi na Arifu ya Mawasiliano. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa uhawilishwaji wa lafudhi ya Kihehe katika Kiswahili sanifu husababisha athari za kifonolojia na kisemantiki. Athari zilizobainika ni udondoshaji, uchopekaji, ubadilishanaji na urefushwaji wa fonimu katika maneno ya Kiswahili sanifu. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa michakato ya udondoshaji, uchopekaji, ubadilishanaji na urefushwaji wa fonimu katika maneno ya Kiswahili sanifu husababisha mabadiliko ya maneno kimatamshi na kimaana.