Utamaduni na Udhibiti wa Nyimbo za Bongo Fleva Nchini Tanzania (2000-2019)
Abstract
Udhibiti wa nyimbo ni changamoto inayowakumba wasanii wa nyimbo za Bongo Fleva. Hali hiyo imechangiwa na kukua kwa tasnia hiyo pamoja na kukua kwa TEHAMA ambapo wasanii wanaweza kujifunza na kuiga kwa haraka mitindo kutoka nje ya utamaduni wa Watanzania pamoja na kufikisha kazi zao kwenye hadhira kwa haraka kabla upungufu wa nyimbo hizo haujagunduliwa. Makala hii imechunguza suala hili kwa kuangalia chimbuko, usuli pamoja na sababu zinazochochea udhibiti wa nyimbo hizo. Data za makala hii zilikusanywa kwa njia ya hojaji na usaili. Wasanii wa Bongo Fleva na viongozi wa taasisi za udhibiti wa sanaa nchini Tanzania walihojiwa. Aidha, baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu waliosomea masuala ya udhibiti wa sanaa walijaza hojaji ili kutoa mawazo yao kuhusu utamaduni na udhibiti. Data zilichambuliwa kwa kuongozwa na Nadharia ya Maadili iliyoasisiwa na Plato. Kutokana na uchunguzi uliofanyika, sababu za kitamaduni za kudhibitiwa kwa nyimbo za Bongo Fleva ni: mosi, kuiga tamaduni za kigeni zilizo kinyume na mila na desturi za Kitanzania. Pili, matumizi ya lugha isiyo na staha katika miktadha mbalimbali pamoja na sababu za kidini. Mjadala wa makala hii umejikita katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000-2019 kutokana na wimbi kubwa la udhibiti wa nyimbo hizo ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.