Kiswahili na Wadau
Fursa na Changamoto kwa Maendeleo Endelevu
Abstract
Lengo la makala hii ni kujadili fursa na changamoto kwa maendeleo endelevu ya lugha ya Kiswahili, hususan baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni - UNESCO kutangaza Siku ya Maalumu ya Kiswahili duniani. Kutangazwa kwa siku hii kunatoa fursa kwa wadau wa Kiswahili katika ngazi zote za kitaifa na kimataifa kujadili masuala mbalimbali yanayohusiana na maendeleo ya Kiswahili. Katika makala hii, pamoja na masuala yaliyolengwa, mwandishi anatoa shukurani zake kwa asasi mbalimbali za kimataifa ambazo zimeshiriki kwa namna tofauti katika mchakato wa kufanikisha hatua ya kutangazwa tarehe 7 Julai kuwa siku maalumu ya Kiswahili duniani. Makala hii inajadili kwa ujumla, majukumu na mchango wa wadau mbalimbali katika maendeleo ya Kiswahili kwa kudokeza fursa na changamoto katika maendeleo hayo. Mtafiti anahitimisha kwa kusisitiza kuwa jukumu la kuendeleza lugha ni la taasisi zote za elimu, hususan vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi. Kutokana na changamoto kubwa ya kifedha, uzalendo uwekwe mbele ili kufanikisha malengo ya kukuza Kiswahili.