Ulinganishi wa Nadharia ya Umbo Upeo na Fonolojia Zalishi katika Uchanganuzi wa Michakato ya Kifonolojia katika Kiswahili
Abstract
Makala hii inahusu ulinganishi wa nadharia za Fonolojia Umbo Upeo na Fonolojia Zalishi katika uchanganuzi wa michakato ya kifonolojia katika Kiswahili. Nadharia hizi mbili zina mielekeo tofauti katika kuchanganua data za kiisimu. Nadharia ya Fonolojia Zalishi hutumia kanuni zinazofanya kazi kihatua katika kukokotoa umbo la ndani kwenda umbo la nje ilhali Nadharia ya Umbo Upeo huzingatia mashartizuizi. Nadharia zilizotumika ni Umbo Upeo na ile ya Fonolojia Zalishi ambapo uchanganuzi umetumia mbinu linganishi. Mashartizuizi yameundwa na mtafiti kutokana na data husika katika kupata matamshi kubalifu. Pia, kanuni zimeundwa na kuonesha ulinganishi wa jinsi mielekeo hii inavyojitofautisha katika kuchanganua michakato ya kifonolojia katika Kiswahili. Imebainika kuwa wakati Nadharia ya Fonolojia Zalishi inabainisha hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kupata umbo la nje kutoka umbo la ndani, mazingira ya utokeaji wa mabadiliko hayo na mabadiliko yenyewe, Nadharia ya Umbo Upeo inahusisha umboghafi na umbotokeo kubalifu kwa kutumia vigezo vinavyowekwa na mashartizuizi katika hatua moja ya ukokotozi. Nadharia ya Umbo Upeo haioneshi kwamba kulikuwa na mazingira fulani yaliyofanya umboghafi likabadilika kuwa umbotokeo fulani.
DOI: http://doi.org/10.56279/jk.v87i1.5