Kategoria za Hofu ya Mwanadamu katika Riwaya ya Kiswahili
Uchunguzi wa Riwaya Teule
Abstract
Mwanadamu huweza kukumbwa na hofu inayojikita katika ufahamu na upembuzi wa masuala mbalimbali yanayomzunguka. Kimsingi, hofu humsababishia mwanadamu huyo kuwa na maamuzi ya kufanya au kutofanya jambo fulani. Kwa asili, mwanadamu ndiye kiumbe mwenye urazini ambaye matendo yake yanaweza kubainisha bayana kuwapo kwa hofu. Waandishi mbalimbali wa kazi za fasihi huwasuka wahusika wenye hofu katika ujenzi wa maudhui lengwa. Hata hivyo, hakuna ithibati dhahiri zinazoonesha kategoria mbalimbali za hofu zinazomkumba mwanadamu kwa kuhusisha na bunilizi za Kiswahili. Kwa mantiki hiyo, makala hii inajadili kategoria tano huku ikijiegemeza katika riwaya za Rosa Mistika (1971) na Ua la Faraja (2004). Kwa ujumla, uteuzi wa riwaya hizi umezingatia kigezo kwamba katika ujenzi wa visa, wahusika wake wanaisawiri hofu kulingana na maudhui lengwa. Data za matokeo haya zilipatikana maktabani kwa kutumia mbinu ya usomaji matini kwa kujiegemeza katika riwaya teule. Vilevile, katika uchunguzi, uchanganuzi na mjadala wa matokeo hayo, misingi ya Nadharia ya Uhalisia imetumika. Matokeo yanaonesha kuwa zipo kategoria mbalimbali za hofu zinazomkumba mwanadamu. Hata hivyo, makala hii imejadili kategoria kuu tano tu, ambazo ni: hofu ya kutokuwa na uwezo wa kuzaa na kulea watoto, hofu ya mahusiano, hofu kuhusu nguvu za Mungu, hofu ya kuyafikia matarajio na hofu ya kifo.