MASIKIDU kama Miviga ya Kuchochea Maendeleo ya Kiswahili
Abstract
Makala hii inachunguza namna Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani – MASIKIDU yanavyoweza kutumiwa kama nyenzo ya kukuza maarifa ya Kiswahili ndani na nje ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, eneo ambalo sehemu kubwa ya wakazi wake wanaweza kuwasiliana kwa Kiswahili. Maadhimisho haya, yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 7 Julai, huwakutanisha wadau mbalimbali wa Kiswahili ambao hujadiliana masuala kadha wa kadha kuhusu lugha ya Kiswahili na utamaduni wake. Kwa hiyo, katika maadhimisho haya, wadau wanaweza kukumbushana na kupeana majukumu ya kuendeleza Kiswahili. Katika makala hii, MASIKIDU yamejadiliwa kama tukio linalochangia kubadilishana maarifa, fikra na mitazamo kuhusu lugha na fasihi ya Kiswahili. Kwa kutumia kiunzi cha miviga ya mpito chenye hatua tatu, yaani (i) mtengo, (ii) mabadiliko, na (iii) ujumuikaji, makala hii inafafanua namna MASIKIDU yanavyoweza kukuza maarifa ya washiriki na kusambaza maarifa hayo kwa wengine. Kwa ujumla, ikiwa kila mdau atashiriki katika MASIKIDU kwa dhamira ya dhati, kuna uwezekano wa maadhimisho haya kuwa kioo muhimu kwa wanagenzi na wanazuoni wa Kiswahili duniani.