Kiswahili na Uandishi, Uchapishaji na Usomaji Nchini Tanzania
Abstract
Makala inaangazia fursa zilizopo katika uandishi na uchapishaji kwa Kiswahili nchini Tanzania, na kuhoji kwa nini mwandishi na mchapishaji hafaidiki kikamilifu na fursa hizo. Ukosefu wa tija katika shughuli hizo umesababisha mdororo mkubwa katika tasnia ya uchapishaji ambayo inajumuisha uandishi, utoaji vitabu, usambazaji na usomaji, na kuwalazimisha waandishi kuacha kuandika, kuacha kuchapisha kazi zao, au kujitafutia mbinu mbadala za kutoa na kusambaza kazi zao. Makala inaeleza kuwa kuzorota kwa usomaji nchini Tanzania ni chanzo kikuu, na pia ni matokeo, ya mdororo huo. Inaelezwa kuwa ufumbuzi wa tatizo hili sharti uanzie katika kutambua uhusiano na mwingiliano uliopo kati ya tasnia ya vitabu, sera ya elimu na mitaala ya lugha. Inasisitizwa kuwa msingi wa maendeleo ya tasnia ya uchapishaji katika mfumo wa ubepari tulio nao ni usomaji; bila kuwa na hadhira pevu ya wasomaji haiwezekani kuwa na tasnia hai ya vitabu. Mitaala ya sasa haiweki uzito katika usomaji; haitambui kwamba, ili kuwa na taifa la wasomaji, usomaji sharti uanzie katika ngazi ya chini kabisa katika shule za elimu ya awali na kuendelezwa hadi shule za msingi na sekondari ili hatimaye litengenezwe taifa la watu wenye tabia na utamaduni wa kusoma. Watu hao ndio watakaokuwa wateja (yaani soko) wa mwandishi na mchapishaji, na ndio watakaoibeba tasnia ya vitabu. Ili kukipata kizazi hicho kipya cha wasomaji, mapendekezo yanatolewa kuhusiana na utoaji wa motisha kwa waandishi, uboreshaji wa mitaala, maktaba za shule na za umma, na uwekezaji katika utoaji na ununuzi wa vitabu vya ziada na ridhaa kwa upande wa serikali na asasi binafsi.