Uzoefu wa Ufundishaji na Ujifunzaji wa Lugha ya Kiswahili nchini Uganda
Abstract
Suala la ufundishaji na ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili nchini Uganda limewashughulisha watalaamu mbalimbali (Kahaika, 2018; Kahaika, 2020; Jjingo, 2020). Wataalamu hao wanadai kuwa Kiswahili ni lugha ya kigeni nchini Uganda hasa kwa kuzingatia matumizi yake finyu katika jamii. Licha ya watalaamu hao kukiri hivyo, bado haijaeleweka namna lugha ya Kiswahili inavyofundishwa nchini Uganda hususani kwa kuzingatia mbinu zitumikazo. Hivyo, makala hii inabainisha namna lugha ya Kiswahili inavyofundishwa nchini huko kwa kuelezea mbinu mbalimbali zinazotumiwa katika ufundishaji na ujifunzaji wake katika ngazi tofautitofauti na changamoto zinazolikumba zoezi zima la ufundishaji na ujifunzaji wa lugha hiyo. Vivyo hivyo, makala hii inafafanua namna lugha ya Kiswahili ilivyofanikiwa nchini Uganda kwa kubainisha nyanja mbalimbali ambako lugha hiyo inatumika. Pia, ili lugha ya Kiswahili ienee zaidi nchini Uganda, makala hii imetoa mapendekezo ambayo yakizingatiwa yatasaidia katika shughuli mbalimbali za ueneaji wa Lugha hiyo. Aidha, makala hii iliongozwa na Nadharia ya Upangaji wa Lugha ya Haugen (1983) inayosisitiza uteuzi wa lugha kisheria na pia utekelezaji wake kupitia shughuli mbalimbali. Data za makala hii zilipatikana kwa kufanya udurusu wa nyaraka mbalimbali zinazopatikana maktabani na mtandaoni pamoja na uzoefu wa mwandishi alionao katika ufundishaji wa lugha ya Kiswahili nchini Uganda.