Maendeleo ya Ufundishaji na Ujifunzaji wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe 2013-2024
Abstract
Kiswahili kilianza kufundishwa katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe mwezi Agosti, mwaka 2013. Ni miaka kumi na mmoja sasa tangu Kiswahili kianzishwe katika chuo hicho. Makala hii inachunguza maendeleo ya ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe. Data za utafiti zilikusanywa kupitia majadiliano ya kundi lengwa na walimu wanaofundisha Kiswahili, upitiaji wa matini hususani zile za sera za lugha katika elimu na usaili wa viongozi wa chuo hususani wakuu wa idara za vitivo vya Chuo Kikuu cha Zimbabwe. Lengo kuu lilikuwa kuchunguza utekelezaji wa sera ya lugha katika elimu ya kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe, maendeleo, changamoto, mahitaji na matarajio. Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba, ingawa Kiswahili kilianzishwa miaka kumi na mmoja iliyopita, bado kuna mambo mengi yanayotakiwa kufanywa ili kustawisha ufundishaji na ujifunzaji wake. Walimu wa Kiswahili ni wachache kuliko idadi ya wanafunzi, vifaa vya kufundishia ni vichache, muda wa kusoma ni mchache na Kiswahili hakisomwi kama digrii. Makala hii imetumia njia saba za utekelezaji wa sera za lugha katika elimu za Kaplan na Baldauf (1997, 2003) kama kiunzi cha nadharia katika kuchunguza maendeleo ya ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe.