Lugha ya Ungonoshaji katika Ushairi wa Bongo Fleva: Mifano kutoka Nyimbo Teule
Abstract
Matumizi ya lugha inayoashiria ungonoshaji yamekuwa yakijitokeza katika nyanja mbalimbali katika jamii zote duniani. Ungonoshaji hujitokeza katika siasa, hotuba, nyimbo hususani katika lugha inayotumika na mazungumzo ya kawaida ya wanajamii (Ngunguti na Mapunda, 2021). Baadhi ya maneno yaliyongonoshwa yanapotumika, wasikilizaji huacha maana ya msingi kwa kupigia chapuo maana ya ziada ya neno husika ambayo mara nyingi huhusishwa na masuala ya ngono. Baadhi ya wataalamu wanalitazama suala la ungonoshaji katika Bongo Fleva kwa namna hasi kwamba ni ukengeushi wa misingi ya maadili ya Mwafrika, jambo ambalo linainyima jamii uhuru wa kujieleza (Ayisi, 1962; Van Pelt, 1971; Karama, 2019; Wanjala, 2020). Makala hii imefafanua matumizi ya lugha ya ungonoshaji katika ushairi wa Bongo Fleva na mifano imetoka katika wimbo wa “Kwangwaru” wa Harmonize na Diamond Platinumz (2018) pamoja na “Baikoko” wa Mbosso na Daimond Platinumz (2020). Data za makala zimepatikana kwa kutumia mbinu ya usikilizaji na utazamaji za nyimbo teule kutoka katika mtandao wa YouTube. Uchambuzi wa data umezingatia mkabala wa kitaamuli na kuongozwa na Nadharia ya Moduli Anuwai. Matokeo yanaonesha kuwa matumizi ya lugha ya ungonoshaji yana dhima ya kufanikisha mawasiliano, kubainisha umuhimu wa mafunzo ya jando na unyago katika jamii na kuonesha ubunifu wa kiutunzi.