Maelekezo kwa Waandishi
Tunapokea miswada ya makala ambazo hazijachapishwa wala kutumwa katika jarida lingine lolote kwa ajili ya kuchapishwa. Miswada inayotumwa lazima izingatie yafuatayo:
- Miswada iwe katika programu ya “word” (DOC, DOCX) na itumwe kwa kutumia anwani za baruapepe zilizobainishwa.
- Vichwa vya makala vinapaswa kuwa vifupi kadiri iwezekanavyo.
- Ikisiri ziandikwe katika aya moja na ziwe na takribani maneno 150 zikijumuisha usuli, tatizo, mbinu, nadharia na matokeo.
- Matini nzima, ikiwa ni pamoja na kichwa, ikisiri, matini kuu, tanichini na marejeleo isizidi maneno 8,000.
- Tumia fonti ya New Times Roman yenye ukubwa wa 12, na maandishi yatenganishwe kwa nafasi mbili kati ya mstari na mstari.
- Tumia “fungua na funga semi” pale unapolazimika tu kufanya hivyo. Unapodondoa matini isiyozidi mistari minne, tumia ritifaa dufu (“...”). Unapodondoa ndani ya matini iliyodondolewa, tumia ritifaa moja (‘...’). Matini inayodondolewa ikizidi mistari minne, tumia mtindo wa dondoo mstatili, yaani anza kuandika dondoo hilo katika mstari mwingine, tumia nafasi moja kati ya mstari na mstari, kazi iwekewe indenti ya sentimeta 1.5 pande zote bila kutumia alama za fungua na funga semi.
- Marejeleo yaandikwe kialfabeti kwa kuanza na jina la mwisho la mwandishi, kama invyoonekana hapa chini:
Vitabu
Massamba, D.P.B. (2002) Historia ya Kiswahili: 50 BK hadi 1500 BK. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Mazrui, A.A. na Mazrui, A.M. (1995) Swahili State and Society: The Political Economy of an African Language. Nairobi: James Currey.
Sura ya Kitabu
Hamisi, A.M. (2008) “Filosofia za Sera za Lugha”. Katika J.G. Kiango (Mh.) Maendeleo ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI. kur. 78-100.
Makala ya Jarida
Ngugi, P.M.Y. (2014) “Fasihi ya Watoto katika Kutekeleza Mahitaji ya Mtoto Kisaikolojia”. Kiswahili, Juz. 77: 170-180.
Collins, E.J. (2018) “Symbolic Arts and Rituals in the African Middle Stone-Age”. Utafiti, Juz. 13(1): 1-22.
Makala ya Jarida la Mkondoni
Wamitila, K.W. (2012) “Uchambuzi wa Tamthilia ya Kaptura la Marx”. Kiswahili, Juz. 78 (1). Inapatikana katika www.swahilijournal.com. Ilisomwa tarehe 12 Juni 2012.
Tasinifu/tazmili Isiyochapishwa
Omari, S. (2009) Tanzanian Hip hop Poetry as Popular Literature. Tasinifu ya Uzamivu (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam.
Gazeti
Duwe, E. (2018) “Zijue Sifa za Kufundisha Kiswahili Nje ya Nchi”. Mwananchi. 16 Oktoba 2018. uk. 13.